Friday, December 18, 2009


HAYA WADAU BLOG YENU IMERUDI UPYA BAADA YA KUTUNDUWAA KWA TAKRIBANI MIAKA MITATU. KWA KIPINDI NILIPOKUWA AFRIKA YA KUSINI TULISHIRIKIANA SANA NA SASA NIPO NYUMBA BONGO NAOMBA USHIRIKIANO WENU KATIKA KUENDELEZA LIBENEKE KAMA MDAU MICHU ANAVYOPENDA KULONGA. KWA MAMBO MBALIMBALI YA KISIASA, UCHUMI NA KIJAMII INGIA KATIKA BLOG HII KILA SIKU.


KARIBUNI SANA WADAU

Wednesday, January 19, 2005

JAMANI MNAOVAA TAI NA SUTI MNAZIJUA SHERIA HIZI.

Vazi la suti mara nyingi humfanya mvaajia aonekane nadhifu na mwenye heshima ndani ya jamii anayoishi hususani kwa akina baba kabwela. Pia kuna uvaaji wa suruali nyepesi, shati jepesi, kiatu cha mchongoko na tai inatangulia mbele watoto wa Dar wanasema vazi la "kipapaa". Vazi hili kutokana na heshima lukuki linazopata kutoka kwa jamii hasa ya makabwela kama nilivyokwisha kusema awali limekuwa likitumika hata na wahalifu kama majambazi na matapeli katika kuwalaghai watu mbalimbali ambao ndio huwa walengwa wa uhalifu wao. Pia vazi hili hupendelewa kutumiwa na viongozi, na mabwana harusi au hata wakurugenzi na mabosi wa mashirika, taasisi, na makampuni mbalimbali.
Lengo langu siku ya leo ni kuwaleteeni sheria zinazotakiwa kuzifuata mtu anapovaa suti la sivyo unaweza kujikuta upo matatani kwa kuvunja moja ya sheria hizo. Sheria zenyewe ni kama ifuatavyo. Unapovaa suti au tai hakikisha huvunji sheria hizi hapa chini:-
1. Ni marufuku kuvaa kandambili au malapa
2. Ni marufuku kuvaa soksi mbovu.
3. Ni marufuku kujisaidia uchochoroni.
4. Ni marufuku kupenga kamasi barabarani.
5. Ni marufuku kupanda daladala.
6. Ni marufuku kuendesha baiskeli au pikipiki.
7. Ni marufuku kucheka cheka hovyo.
8. Ni marufuku kuomba change dukani.
9. Ni marufuku kubeba mfuko wa plastiki maarufu kama rambo
10. Ni marufuku kuingia kwenye kibanda cha simu.
11. Ni marufuku kula magengeni.
12. Ni marufuku kuonekana unatafuna barabarani.
13. Ni marufuku kutembea na pesa za sarafu mifukoni mwako.
12. Ni marufuku kulia hata kama umeletewa taarifa ya msiba.
14. Ni marufuku kupiga miruzi.
15. Ni marufuku kuonekana unatoka mijasho kama unasukuma mkokoteni.
16. Ni marufuku kuongea kwa kelele.
17. Ni marufuku kunywa chai au kahawa kwa kutumia kikombe cha plastiki.
18. Ni marufuku kutembea kwa miguu.
19. Ni marufuku kukimbia.
20. Ni marufuku kunuka mdomo wala kikwapa hili kosa kubwa sana na hukumu yake mpaka mbinguni ipo.
21. Ni marufuku kusema uongo.
22. Ni marufuku kuonekana umekasirika unatakiwa uwe na uso uliokunjuka.
23. Ni marufuku kumchapa mtoto.
24. Ni marufuku kusababisha ubishi au mjadala uso na maana.

Kwa leo tuanamaliza na sheria za suti na tai siku nyingine tutawaletea masharti ya kujiunga na chuo na vibaka huko maeneo ya uwanja wa fisi jijini Dsm.

Thursday, January 06, 2005

BLOG ZA WATANZANIA

Heri ya mwaka mpya Watanzania wenzangu popote mlipo Duniani. Ni matumaini yangu kwamba mmeuanza vema mwaka 2005, huku kila mmoja akiwa na lake kichwani hasa malengo mazuri kwa mwaka huu mbichi wa 2005. Napenda kutoa shukurani za dhati kwa wasomaji wangu wote ambao walikuwa sambamba na mimi katika makala zangu mbalimbali za mwaka 2004 pia napenda kutoa shukurani kwa wasomaji wote ambao walikuwa wakinitumia maoni yao na wale wote walionisaidia kwa namna moja ama nyingine katika kufanikisha maendeleo ya blogu hii ya kiswahili kwa lengo la kupashana habari kupitia teknolojia hii ya kisasa ya mawasiliano.Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitatoa shukrani za pekee kwa bwana Ndesanjo Macha, mtanzania mwenzetu aishiye marekani kule kwa mbabe Joji Kichaka.
Hizi ni baadhi ya blogu za watanzania waishio ndani na nje ya Tanzania furahia.blogspot.com, jikomboe.blogspot.com , mkini.blogspot.com pia zipo blog nyingine nyingi ambazo nitawawekea wakati mwingine.